SOMO LA MALEZI CHUO CHA UALIMU

TOTO

                                                    YALIYOMO

Shukrani……………………………………………………………………………………………………………………………………
Utangulizi………………………………………………………………………………………………………………………………..
Sura ya Kwanza: Mtazamo wa Elimu ya Awali……………………………………………………………………………
Somo La Kwanza:Dhana ya elimu ya awali na maendeleo yake…………………………………………..
Somo La pili: Nadharia ya elimu ya awali………………………………………………………………………

Sura ya Pili: Mtaala Wa Elimu Awali……………………………………………………………………………………….
Somo la kwanza: Dhana ya Mtaala Wa Elimu ya awali……………………………………………………
Somo la Pili: Utayarishaji,Uchambuzi na Utekelezaji wa Mtaala Wa elimu ya Awali………….

Sura Ya Tatu: Mbinu za kufundishia na kujifunzia elimu ya awali……………………………………………..
Somo la kwanza: Dhana ya njia,Mbinu za kufundishia na kujifunzia elimu ya awali…………..
Somo la Pili:Mbinu za kufundishia na kujifunzia………………………………………………………….

Sura Ya Nne: Ukuaji wa mtoto……………………………………………………………………………………………….
Somo la kwanza:Dhana ya ukuaji wa mtoto
Somo la pili: utunzaji wa mtoto…………………………………………………………………. ……………….

Sura Ya Tano:Kujifunza kwa mtoto………………………………………………………………………………………………..
Somo la kwanza:Dhana ya kujifunza kwa mtoto…………………………………………………………………
Somo la pili:Nadharia ya kujifunza kwa mtoto……………………………………………………………..
Somo la Tatu:jinsi ya kuwatambua na kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalumu ya kujifunza

Sura Ya Sita: Afya ya Mtoto…………………………………………………………………………………………….

          Somo la kwanza: Dhana ya Afya  na lishe bora…………………………………………………………

           Somo la pili:Huduma ya kwanza…………………………………………………………………………….

           Somo la tatu:Kisanduku cha huduma ya kwanza……………………………………………………..

            Somo la Nne: Huduma za afya kwa mtoto…………………………………………………………….

            Somo la Tano:Magonjwa ya watoto……………………………………………………………………

Sura Ya saba:Mawasiliano katika utoaji wa elimu ya awali……………………………………………………
Somo la kwanza:Mawasiliano…………………………………………………………………………………

Sura Ya Nane: Uongozi na utawala katika elimu ya awali……………………………………………………….
Somo la kwanza:Uendeshaji wa shule za awali……………………………………………………………

Sura Ya Tisa:Mazoezi ya kufundisha…………………………………………………………………………………….
Somo la kwanza:Dhana na umuhimu wa mazoezi ya kufundisha……………………………………..

Sura ya Kumi:Uchunguzi Wa mtoto……………………………………………………………………………….
Somo la kwanza:Dhana na umuhimu wa uchunguzi wa mtoto…………………………………..
Somo la pili:Njia za kufanya uchunguzi wa mtoto……………………………………………………
Somo la Tatu:Matumizi Ya matokeo ya Uchunguzi wa mtoto…………………………………….

Rejea

Agakhan   Education  Service Tanzania (1990)Mwongozo wa mitaala ya waalimu wa shule za
Awali Dar es Salaam

Decker   (1988) Planning and Administering Early Childhood Programs:Macmillan Publishing
House, New york.

NACECE (2002) Early Childhood Development Manual for Caregivers

NACECE (1999)Guidelines for Early Childhood Development  in Kenya,Nairobi

URT   (1995) Sera ya Elimu na Mafunzo, Dar es salaam

Regional Training and Resource Centre,(2001)Child Development(A Module for Training of
Early Childhood Education Teachers and Categories, Nairobi.

Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (I987)Malezi ya Watoto wadogo ,Dar es Salaam.

Wizara ya Elimu na Utamaduni (1993)Mwongozo wa Elimu ya awali:Dar es Salaam

UTANGULIZI

Mwalimu wa elimu ya awali anatakiwa awe na msingi mzuri wa kitaaluma na kitaalamu ili  aweze kutoa elimu iliyobora na kukidhi mahitaji ya watoto katika kujifunza.Aidha ufundishaji na ujifunz
aji  wa watoto hutokea katika njia mbalimbali rasmi na zisizo rasmi hivyo mwalimu wa shule ya- awali anahitaaji maarifa na stadi za nyongeza ili kuwa mbunifu na mnyumbufu ili kila mtoto apate
msaada unaostahili.Moduli hii imeandaliwa kwa ajili ya waalimu wanafunzi wanaosomea ualimu- ngazi ya cheti walio vyuoni na wanapokuwa nje ya vyuo.

Moduli hii ya malezi ya Elimu ya Awali inajumla ya sura kumi kama ifuatavyo:

 1. Mtazamo wa elimu ya awali.
 2. Mtaala wa elimu ya awali.
 3. Mbinu za kufundishia na kujifunzia elimu ya awali
 4. Ukuaji wa mtoto.
 5. Kujifunza kwa mtoto.
 6. Afya ya mtoto
 7. Mawasiliano katika utoaji wa elim ya awali
 8. Uongozi na utawala katika elimu ya awali.
 9. Mazoezi ya kufundisha
 10. Uchunguzi wa mtoto.

Kila sura imegawanywa katika masomo kadhaa kulingana na idadi ya mada ndogo zinazofafanu-a sura hiyo. Muduli hii imeandaliwa kaika muundo unaomwezesha mwanachuo kusoma mwenyew
e  na kupatiwa msaada wa ufafanuzi katika maeneo yenye kuhitaji msaada zaidi kutoka kwa mkuf
unzi darasani.

vile vile moduli hii pia inamwezesha mkufunzi kujua namna gani  anaweza kulifundisha somo hili
kwa kuzingatia mbinu na njia za mfano zilizopendekezwa.

Ni matuani yangu kuwa sote tutashirikiana ili kuhakikisha kwamba tunatimiza malengo yaliotule
ta hapa SINGACHINI.Kumbuka kusoma sio lelemama,kusoma kunahitaji nidhamu ya hali ya juu
na hamu ya kutaka kufahamu kwa yule mwenye kusoma.

Mkufunzi wa somo la Malezi Elimu ya Awali  anawatakia masomo mema na  mafanikio katika kusoma ili muwe Waalimu bora na sio bora Waalimu ili mkalitumikie Taifa la Tanzania.

MTAZAMO WA ELIMU YA AWALI
Elimu ya awali ni elimu ambayo inatolewa kwa ajili ya watoto  wenye umri unaoanzia miaka 5 hadi 6.Elimu hii iatolewa kwa watoto ili kuwajengea msingi mzuri wa kielimu,ambapo mtoto anapomaliza elimu hii anaendelea kujiunga na elimu ya msingi.

Elimu ya awali inatolewa kwa watoto wadogo ili waweze kujifunza katika umri huo mambo mbalimbali ya kijamii,kielimu na kiutamaduni ili kuwajengea tabia na mwenendo bora kulingana namwelekeo wa jamii na nchi kwa ujumla.

Katika shule hizi watoto hujifunza kwa kiasi kusoma,kuandika na kuhesabu.Wakiwa shuleni watoto hujifunza ushirikiano na watu wengine,tabia njema kazi za mikono na mambo mengine ambayo huwasadia katika makuzi yao.

UMUHIMU WA ELIMU YA AWALI
Utafiti umeonyesha kuwa utoji wa elimu bora na stadi mbalimbali katika umri wa miaka o-6 huchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mtoto katika maisha yake yote. Mtaalamu Myres alithibitisha kuwa mtoto anayeanza darasa la kwanza baada ya kupitia elimu ya awali huweza kujifunza na kufundishwa vizuri zaidi.Aidha  mtaalamu huyo pia alithibitisha kuwa utoro na kurudi rudia  madarasa hupungua ingawa kwa upande mwingine utoro ni kama tabia ya mtoto mwenyewe inayoweza kuchangiwa na mazingira yaliyomzunguka.Ili kuandaa mazingira ya utoaji wa elimu bora  katika ngazi ya awali,mambo yafuatayo ni muhimu kuzingatia baina ya waalimu na wazazi.

 • Kutoa malezi bora kwa watoto kwa kuzingatia lishe bora.
 • Kukuza maendeleo ya jamii yanayomlenga mtoto katika makuzi yake
 • Kutoa huduma za msingi kwa watoto katia shule za awali ili kuwawezesha kupata maarifa bora zaidi na kuwajengea misingi mizuri ya ufahamu
 • Kuelimisha kuhusu umuhimu wa elimu ya awali ili k uweza kuwapatia watoto elimu hii katika kuwajengea msingi mzuri wa elimu.Watoto pia washirikishwe katika mchakato wa kujifunza kwani wao ndio wahusika wakuu.

BAADHI YA UMUHIMU WA ELIMU YA AWALI NI KAMA UFUATAVYO

 • Kuwapa watoto nafasi ya kucheza na kujifunza kutoka kwa watoto wengine katika jamii yao.
 • Kuwaandaa watoto kwa ajili ya kujiunga na elimu ya msingi.
 • Kuchochea maendeleo ya makuzi ya watoto kimwili,kimaono, kijamii,kiakili, na kihaiba.
 • Kuwaongezea watoto maarifa na uwezo wa kujifunza.
 • Shule za awali pia ni vituo vya malezi  ya watoto  na hivyo kawawezesha wazazi kufanya kazi zingine wakati watoto hao wakiwa shuleni.
 • Shule za elimu ya awali husaidia pia katika kubainisha watoto wenye mahitaji maalumu ya kujifunza  kama vile wenye mtatizo ya kiakili,wasiosikia,wasioona,pamoja na matatizo mengine

ambayo huathiri mwenendo wa kujifunza kwa watoto.Ubainishaji wa matatizo haya mapema huwasaidia watoto kuweza kupatiwa msaada mapema kabla tatizo halijawa kubwa zaidi.Pia taarifa hizi husaidia  serikali kubuni mipango ya kuwasaidia watoto hawa mapema.

HISTORIA NA MAENDELEO YAELIMU YA AWALI NCHINI TANZANIA

Elimu ya awali katika Tanzania bado haijapiga hatua kubwa, hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na kukuwa kwa kasi kwa uanzishwaji wa shule za awali.Elimu ya awali pia haijakua sana katika sehemu za vijijini ambako ni sehemu chache mno zenye shule za awali kutokana na upungufu wa walimu na mwamko duni wa wazazi kuhusu elimu hiyo.

Uamuzi wa hivi karibuni  wa serikali wa kuwa  na shule ya awali  katika kila shule ya msingi ya serikali huenda ukachochea zaidi  ukuaji wa elimu hiyo katika siku za hivi karibuni.

Elimu ya awali ilianza mwaka 1940 wakati wa kipindi cha ukoloni.Shule zilianzishwa kwa lengo la kutoa
elimu kwa watoto wadogo.Wakati huo elimu ya awali ilitolewa zaidi na taasisi za kidini hasa zile za kikristo na serikali ya kikoloni kwa watoto wa tabaka fulani tu.Ipo elimu pia iliyotolewa na wenyeji kwa kila jamii husika,elimu hiyo ilijulikana kama elimu ya asili ambayo ilitolewa katika jamii ile mtoto alipozaliwa.

Baada ya uhuru mwaka 1961 serikali ilitoa nafasi kwa taasisi mbalimbali ili kuanzisha na kutoa elimu ya awali kwa kufuata miongozo iliyowekwa.

Mwaka 1982  ripoti ya Tume ya Raisi ilipendekeza kuwa elimu ya awali iingizwe katika mfumo rasmi wa elimu,Wizara ya Elimu na Utamaduni ilipendekezwa iandae miongozo na vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kutoa mafunzo kwa waalimu wa elimu ya awali.

Miongozo ilitayarishwa mwaka 1991 na Wizara ya elimu na utamaduni lakini kwa kuwa hakukuwa na chombo cha kufuatilia utekelezaji wake shule nyingi zilitoa elimu ya awali bila kuzingatia viwango vinavyostahili.

Mwaka 1995 Sera ya Elimu na Mafunzo ilitolewa na kuelekeza kuwa elimu ilimu ya awali itatolewa kwa watoto wa miaka 5-6 na itasimamiwa na Wizara Ya Elimu na Utamaduni.Aidha sera hii inaelekeza kuwa wajibu wa wizara ya Elimu na Utamaduni ni kutoa maelekezo ya kisera , kutoa mafunzo kwa shule hizo na hatimaye serikali za mitaa,mashirika binafsi yaanzishe na kuendesha shule za awali.Serikali pia imeweka msisitizo wa kuanzishwa kwa shule za awali baada ya kuona idadi ya watoto ni kubwa ikilinganishwa na shule zilizopo.Hata hivyo kumekuwa na ongezeko la shule za awali katika mikoa mbalimbali ingawa bado haikidhi mahitaji.

NADHARIA MBAlIMBALI  ZA ELIMU YA AWALI
MAWAZO YA WANAFALSAFA JUU YA ELIMU YA AWALI

MARIA MONTESSORI(1870- 1952)

Alizaliwa Italia alikuwa mwanamke wa kwanza nchini Italia kuwa daktari wa magonjwa ya watoto na magonjwa ya akili.Katika ugunduzi wake alingundua kuwa watoto waliovia akili wanaweza kufunzwa kwa kutumia vifaa vya kuchezea wanavyovipenda.Aliamini kuwa tatizo la kuvia akili ni la kielimu na sio la tiba.

Montessori aliamini kuwa elimu ya mtoto ni lazima ianze mapema sana kwa sababu umri wa mtoto  kati ya kuzaliwa  hadi miaka sita ni muhimu sana kwa ujenzi wa haiba yake.

Ili mtoto aweze kujifunza kwa ufanisi zaidi ni muhimu kwa mzazi au mwalimu kutumia michezo na vitendo vinginevyo katika kufundisha,hii itamsaidia mtoto katika kujifunza kujifunzia stadi mbalimbali za utendaji .

Pia alipendekeza mwalimu atumie vifaa vingi katika ufundishaji,vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokuza tabia ya udadisi na ugunduzi,vinavyompa nafasi ya utendaji na vinavyomwezesha kufanya majarabio,kutatua vikwazo,ujasiri,kuuliza na kujibu maswali,kupenda kufaulu, kujiendeleza na kumpa msukumo wa kujitegemea katika utendaji.

Alitaka watoto wenyewe wajishughulishe kikamilifu katika kila kitu wanachofanya katika mazingira yaliyo tayarishwa  vizuri na mwalimu kwa kuwapatia  vifaa muhimu vinavyo hitajiwa.

Alibuni michezo ya kujifunzia,alitumia vifaa vya kuchunguza ambavyo humpatia mtoto maarifa  na hapo hapo kukuza stadi wakati anapovichezea.Alifanya kazi ya kujifunza iwe ni rahisi na ya kufurahisha kwa kutumia vifaa vya kuchezea,vifaa hivyo vya kujifunzia vinaweza kutengenezwa kwa mti, vipande vya nguo,chuma,au karatasi nene.

Kuhusu vyumba/nyumba za madarasa ya watoto alipndekeza igawanywe katika vyumba vingi na kila chumba kiwe kwa ajili ya kufanyia shughuli maalumu tofauti, watoto wawe huru kutembea na kuingia kila chumba  wakitakacho bila kizuizi.

Wanafunzi wajifunze kwa kushirikiana na hali inayotakiwa mle vyumbani iwe ya kuheshimu haki na kazi za kila mtu.Watoto wadogo wajifunze kutoka kwa wenzao walio wakubwa.,vifaa vilivyomo katika nyumba kwa mfano viti vya kukalia viwe vidogo kama walivyo watoto wenyewe.

MARIA MONTESSORI   anajulikana sana kwa kuwa mtu aliyeanzisha njia ya kuwafundisha watoto wadogo.Njia yake ya kufundishia watoto wadogo aliigawa katika sehemu kuu zifuatazo

 1. Elimu inayohusu ukuzaji wa stadi mbalimbali za misuri ya watoto,elimu hii ni nzuri kwa kumsaidia mtoto aweze kukuza stadi zake na kufikia upeo wa juu katika kutumia viungo vyake vya mwili,ili kufikia hali hii wanafunzi wafanye mazoezi mbalimbali ya kutembea na kupumua.mazoezi haya humfanya matoto awe na umbo zuri na pi humsaidia kujenga mazoea ya kutumia lugha vizuri. Pia alitumia elimu ya aina hii ya mazoezi yanayohusiana na maisha ya kila siku ya mtoto kwa mfano usafi wa mwili,usafi wa mazingira ya ndani na ya nje.
 2. Elimu inayohusu ukuzaji wa milango ya fahamu,mazoezi aliyoyapendekeza kwa watoto ni yale ya kuwasaidia watoto kuweza kutofautisha  kati ya uwingi na ubora wa kitu,mazoezi yanayotumiwa  katika elimu hii ni yale ya kuona na kusikia.
 3. Elimu inayohusu weledi,mazoezi ya kuwapa wanafunzi ni yale ya kumtayarisha mtoto kusoma kuandika na kuhesabu kwa mfano mtoto huanza kugusa, kuangalia,kuandika na hatimaye kusoma .Vifaa ni vya lazima sana kwa kukuza elimu ya aina hii,vifaa hivyo ni kama vile shanga za rangi mbalimbali, vizibo vya chupa,vipande vya miti vilivyoandikwa namba,alfabeti zinazoweza kusogezwa au mbegu za mimea,

Kutokana na ufundishaji wake wa watoto wadogo MARIA MONTESSORI  alipendekeza na kusisitiza mambo muhimu yafuatayo

 • Watoto wafundishwe kwa njia ya michezo
 • Watoto wapewe fursa ya kuchagua michezo na hata vifaa vya kuchezea
 • Watoto wapatiwe fursa ya kuwa huru

JEAN JACQUES ROSSEAU (1712-1778)

Alizaliwa mwaka 1712 katika mji wa Geneva huko Uswisi ambako alipata mafunzo yake ya awali kutoka kwa baba yake na baadae kutoka kwa mkufunzi aliye kuwa ameajiliwa kumfundisha.Kitabu Emili ndicho hasa kilichoeleza mawazo yake juu ya malezi ya watoto.

ROSSEAU alikuwa na mwelekeo wa kuamini kuwa kwa asili watoto huzaliwa na tabia nzuri na kwamba mazingira  huwafanya wawe na tabia mbaya.Alisisitiza njia bora ya kuwaelimisha  watoto ni kuwaweka katika hali ya asili ambayo itamwezesha kukuza tabia,silika zao za uwezo wao bila kuathiriwa na mazingira

Aligawanya maisha ya mtoto katika hatua nne

 1. Hatua ya kwanza ni ya utoto mchanga, huu ni wakati mtoto anapojenga mazoea na tabia njema ni wakati unao faa kumwongoza mtoto kutawala maono yake
 2. Hatua ya pili ni mtoto mdogo,huu ni wakati wa kujifunza namna ya kutumia milango yake ya maarifa
 3. Hatua ya tatu ni mwanzo wa uvulana au usichana hiki ni kipindi cha akili mtoto anapotumia akili yake juu ya vitendo anavyofanya
 4. Kipindi cha nne ni uvulana au usichana mpevu(baada ya miaka 15)hiki ni kipindi cha fikra za kiroho,hapo mtoto anatambua hasa mema na mabaya

ROSSEAU alieleza umuhimu wa mtoto kuwa kitovu cha elimu ili kumpa hali nzuri ya maisha.Alisisitiza kuwa elimu lazima imsaidie mtoto huyo kuwa huru na mwenye furaha,elimu imsaidie mtoto kukuza haiba nzuri ili elimu iweze kufikia malengo haya lazima itolewe kufuatana na hali na hatua za kukua kwa mtoto.

Mtoto afundishwe jinsi ya kujifunza na jinsi ya kutatua matatizo katika mazingira malimbali,Alisisitiza kuwa elimu ni haki ya watoto wote ni chombo kinachoweza kuyatawala mazingira ya mtoto.

Alishauri kuwa ufundishaji  uende sambamba na hatua za ukuaji wa mtoto.uzingatie upevu na utayari wa mtoto katika kujifunza.

Njia bora za kufundishia ni zile zinazomsaidia mtoto kutumia milango mingi ya fahamu inavyowezekana ili kufanikiwa katika jambo hili mwalimu atumie zana za kufundishia hasa kwa kutumia vitu halisi.
Katika ufundishaji mwalimu atumie njia zitakazo mwezesha mwanafunzi kujifunza kwa vitendo.
Ili watoto wawezekujifunza kwa urahisi mwalimu aanze kufundisha mambo yanayofahamika kuelekea mambo yasiyofahamika.

Falsafa ya ROSSEAU  juu ya elimu inafanana na falsafa ya elimu Tanzania .
Rosseau alikazia kuwa mitaala na ufundishaji imlenge mwanafunzi yaani mwanafunzi awe msingi wa  kuzingatiwa katika elimu,kwenye kujitegemea jambo ambalo limesistizwa pia kwa mfano elimu ya kila ngazi inasisitizwa ijitosheleze yaani mwanafunzi amalizapo ngazi moja ya elimu aweze kujitegemea.

Kufuatana na Rosseau elimu lazima izingatie mahitaji ya maadili,katika falsafa ya elimu ya kujitegemea ufundishaji wa maadili umezingatiwa kwa kuwafundisha wanafunzi masomo ya siasa na dini.

JOHN DEWEY

John Dewey alizaliwa mwaka 1859  huko Vermont,Marekani na alifariki mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka 93.Dewey aliandika mengi na kufanya mengi yaliyo mfanya atambuliwe na dunia kuwa mwamba katika utaalamu wa falsafa na pia kuwa mwlimu hodali na mtu aliye kuza nadharia inayohusu malezi ya watoto.

Kutokana na kazi ya Dewey zilianzishwa shule zilijulikana kama  shule za maendeleo, na malezi yaliyo tolewa yakaitwa malezi ya maendeleo,akiwa Michigan Dewey alianzisha kituo cha watoto wadogo alichokiita shule ya maabara  mwaka 1896 alikusudia shule hiyo itoe nafasi ya kufanya utafiti na majaribio juu ya namna ya kujifunza.

Dewey alisisitiza kuwa elimu haiwezi kutengwa na jamii kwa hali hiyo basi, elimu ni njia ambayo jamii huitumia katika kulinda kuendeleza na kuhifadhi utamaduni wake.Madhumuni ya elimu basi ni kutayarisha na kutoa raia walio bora na wanaoweza kuitumikia jamii yao kikamilifu.

Dewey aliamini kuwa katika kutenda au kufanya shughuli fulani wanafunzi wanaweza kuelewa mambo vizuri zaidi.Alisisitiza kuwa maarifa hupatikana kutokana na shughuli wazifanyazo watoto.

Kuhusu suala la kujifunza Dewey alitaja mambo ambayo ni muhimu kuzingatia wakati wa kumfundisha mtoto.Mambo hayo ni haya yafuatayo

 1. Mwanafunzi mwenyewe lazima awe katika mazingira  halisi ya aina ya uzoefu anaotakiwa kupata
 2. Lazima kuweko na tatizo la kweli linaloamsha na kuchochea  mawazo na ari ya mwanafunzi ya kutatua matatizo.
 3. Mwanafunzi mwenyewe lazima afanye uchunguzi na atafute au akusanye data za kumsaidia katika kulitatua tatizo lake.
 4. Ni lazima ajaribu kutafuta ufumbuzi mbalimbali wa tatizo hilo.
 5. Ni lazima apate muda wa kufanya majaribio kuona kama mawazo au dhanio alizozipata ni kweli zinaweza  kuwa na uthibitsho wowote

Dewey alilisisitiza kuwa shule iwe kaya njema ambamo mtoto atafundishwa maadili yote ya jumuiya yake,shule iwe kaya njema ambamo mtoto atafundishwa maadili yote ya jumuia yake shule imjenge mtoto kimwili kiakili na kitabia.

  Dewey hakuona umuhimu wa mgawanyo wa mafunzo katika masomo kama ilivyo hivi sasa kwa mfano,historia, Jiografia,hisabati,na sayansi bali alihimiza kuwa masomo yote yatolewayo hapana budi yazingatie

 • Shughuli anazofanya mtoto mwenywe
 • Shauku aliyo nayo mtoto wakati wa kujifunza
 • Matatizo anayopambana nayo
 • Mahitaji yake ya kila siku

FRIEDRICH  FROEBEL

Froebel anashika nafasi ya pekee kati ya wataalamu wa mambo ya malezi.Ijapokuwa mawazo yake makuu yalifanana na yale ambayo ROSSEAU alikuwa amekwisha kuyaandika.

Alizaliwa ujerumani mwaka 1782 katika kijiji kilichokuwa katika msitu wa Turingia.Akiwa kijana bado alifanya kazi chini ya uangalizi wa Bwana misitu,na kwa nafasi hiyo alijipatia moyo wa kupenda uoto wa asili juu ya sura ya nchi,na pia kupenda maumbile ya asili ya nchi.

Baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Jena ambapo kaka yake alikuwa pia akisoma.hapo aliendeleza ujuzi wake wa mambo ya sayansi na hisabati.Ulimwengu mzima ulilazimika kumsikiliza Froebel kwa makini kwa sababu kuu mbili

 1. Kwanza Froebel alikuwa mwalimu maarufu sana ambaye alijenga shule yake mwenyewe na katika shule hiyo akatekeleza kwa matendo yale aliyo kuwa ameyanena kwa maandishi.
 2. Pili matokeo ya mafanikio ya shule hiyo yaliwatia moto wafuasi wake,nao wakayachukua mawazo ya mwalimu wao kwa moyo wa kitume,wakayaeneza katika sehemu mbalimbali za dunia,liliundwa hata shirika la kimataifa la kueneza mawazo ya froebe,shirika ambalo lilisaidiwa na kuungwa mkono na matajiri wengi.

Sifa kuu ya Froebel imo hasa katika kuzua wazo la kuwa na shule za Chekechea (kindergarten)jina hili la Kindergarten ambalo lina maana ya “bustani ya watoto”  ndilo hasa lililoeleza imani na msimamo wa Froebel juu ya malezi.Yeye alimlinganisha mtoto na mmea mchanga,na kazi ya mwalimu akailinganisha na kazi ya mkulima bustani,ambaye wajibu wake ni kutengeneza mazingira yanayofaa illi mmea ukue wenyewe hata kufikia kikomo chake.

Mawazo yake kuhusiana na elimu na jinsi ya kumuandaa mtoto kielimu ni haya yafuatayo:

Froebel alipendekeza pawe na umoja katika mambo yanayofundishwa na kutaka tuepuke hatari ya kuyagawa masomo katika sehemu ndogondogo zisizohusiana kwa mfano yeye alihimiza kuwa mitaala ya masomo ionyeshe umoja.Aliwalaumu pia waalimu wa vyuo vikuu ambao walikuwa wameligawa somo la malezi katika sehemu nyingi ili waandike vitabu.

Alisema pia katika shughuli ya malezi uhuru wa mtoto ni muhimu kuzingatiwe ,
“ sisi binadamu tunapotunza mimea na wanyama tunawaachia nafasi ya kujimudu na pia muda wa kukua,tikijua kuwa kwa kufanya hivyo mimea yetu na wanyama wetu watakuwa sawa sawa kdili ya asili ya kukua:tunawapa fursa ya kupumzika na hatuyaingilii maisha yao kinguvunguvu,wala hutuwafanyi vitendo vyovyote vitavyozuia kukua kwao.Lakini mtoto wa binadamu tunamfanya kama kipande cha nta au donge la udongo ambalo tunaweza kuligeuza kuwa umbo lolote tulitakalo,kwa nini hatutaki kujifunza kutokana na jinsi mama dunia anavyokuza viumbe vyake!
Katika hili pia alisema kazi ya mlezi/mwalimu ni kumfuata na kumlinda mtoto,isiwe kazi ya kumwamuru,kumkatia mashauri au kuyaingilia maisha yake.

Jambo lingine Froebel anafikiri kuwa ni muhimu kwa kila mlezi kuhakikisha kwamba mahitaji ya mtoto ya akili, vionjo na mwili yanatimilizwa katika kila kipindi cha kukua kwake.Ili maendeleo ya mtoto yaweze kutimilika katika kipindi fulani cha kukua ni lazima maendeleo ya kipindi kilichotangulia yawe yametimilika kwanza,ni lazima mwalimu afahamu vizuri tabia na mahitaji ya watoto katika kila kipindi cha kukua kwao.

Froebel pia alitlilia mkazo vitendo kuliko nadharia vitu vya kuchezea kuliko vitabu,stadi za mikono kuliko stadi za akili mawazo yake yalifanana na yale ya ROSSEAU katika hili,lakini pia Froebel alitilia mkazo ujengaji wa uhusiano mwema kati ya watoto jambo ambalo ROSSEAU hakutilia maanani.

Jambo lingine kubwa katika Mawazo ya Froebel linaoandamana na mawazo yake juu ya kukua kwa watoto,ni kucheza,anasema kuwa kucheza ni njia pekee inayokuza uwezo wa watoto kujifunza.Anasema
“kucheza ndilo jambo bora kabisa katika maendeleo ya mtoto,kucheza ni kujieleza kwa mawazo na vionjo ambako hutokana na msukumo wa mtoto ulio ndani ya mtoto.Hii ndio maana ya neno kucheza”

Anaendelea kusema kwamba katika kucheza mtoto hukuza vipawa vitakavyojionyesha zaidi katika utu uzima,mtoto achezapo hujenga misingi ya tabia yake ya baadaye iwapo atakuwa mtu mpole au mkatili,mkarimu au mwenye choyo,mvivu au mwenye bidii,mpumbavu au mwerevu,mharibifu au mtunzaji vitu.

Pia Froebel anazungumzia jambo alilotilia mkazo ROSSEAU yaani ubora wa kumshughulisha mtoto wakati anapojifunza(shughuli ya mtoto mwenyewe).Alionyesha pia faida ya uongozi wa mwalimu,na faida ya mtoto kujifunza pamoja katika vikundi vidogovidogo,au pengine kujifunza pamoja wakiwa darasa zima,alipendekeza pawe na uwiano wa kufaa kati ya kumwacha mtoto  kujishughulisha peke yake,na kuongozwa na mwalimu,na pia kati ya kumwacha mtoto ajifunze peke yake na kumshirikisha na wenzake.

Kwa kweli madhumuni ya njia za kujifunzia alizopendekeza Froebel yalikuwa kuwapa watoto uzoefu wa kweli wa kisayansi,kwa kuanzia na upekuzi wa mambo yaliyowapendeza watoto wenyewe.Mafunzo juu ya maumbile ya asili,kama vile sura ya nchi,mimea na wanyama yalipewa nafasi kubwa katika ratiba ya masomo,na mara nyingi masomo yalifanywa nje ya darasa ili watoto waweze kuyaelewa mazingira yao.

Ijapokuwa Froebel alikazia jambo hilo la kujifunza kwa vitendo alionya pia kwamba katika kufanya vitendo vya aina mbalimbali watoto wasilazimishwe kushindana kwani si jambo zuri kumlinganisha mtoto mmoja na watoto wengine.,badala yake kila mtoto ashindane na yeye mwenyewe yaani kila mara ajaribu kufanya vizuri kuliko alivyofanya mwanzo.

UCHAMBUZI WA VIFAA VYA MTAALA WA ELIMU YA AWALI.

Mtaala wa elimu ya awali hauna tofauti kubwa na ule wa shule ya msingi,isipokuwa katika elimu ya awali wanatumia muhtasari wa vitendo vya masomo na sio muhtasari wa somo kama ilivyo katika shule ya msingi.Ni muhimu kujua vifaa vya mtaala wa elimu na jinsi ya kuvitumia katika ufundishaji wa elimu ya awali.

AINA ZA VIFAA VYA  MTAALA WA ELIMU YA AWALI.

Muhtasari wa elimu ya awali,chati inayoonyesha vifaa mbalimbali vya kufundishia elimu ya awali,kiongozi cha mwalimu,vitabu vya kiada na viada.

Mtaala wa elimu ya awali unajumuisha vifaa mbalimbali kama vile muhtasari wa vitendo vya masomo ambao unaonyesha mada kuu na mada ndogo mbalimbali na malengo ya kufundishia mada hizo,vitabu vya kiada,ziada na kiongozi cha mwalimu.

Mwalimu wa darasa la awali atatumia muhtasari wa vitendo vya masomo kuaandaa azimio la kazi na andalio la vitendo vya masomo,pia anatakiwa kujua mbinu mbalimbali za kufundishia elimu ya awali na vifaa vitakavyotumika kufundisha mada za vitendo mbalimbali vya masomo.

Mwalimu wa awali pia anatakiwa kubuni na kutengeneza  vifaa mbalimbali vya kufundishia  na kujifunzia ambavyo vinapatikana katika mazingira yake.Vifaa hivyo vitamsaidia katika uwasilishaji wa mada mbalimbali za vitendo vya masomo darasani  na pia nje ya darasa.

Umuhimu wa kujua vifaa vya mtaala ni kumsaidia mwalimu wa elimu ya awali kupanga masomo yake vizuri na kufundisha kwa ufanisi kwa kufuata mpangilio alioupanga.Pia vinamsaidia kujua ni vifaa/Zana gani aandae kwa ajili ya kufundishia mada mbalimbali.
Muhtasari wa Vitendo vya Masomo.
Muhtasari wa elimu ya awali ni tofauti na ile ya shule ya msingi kwa sababu umeundwa kwa vitendo vya masomo mbalimbali.Ni rahisi zaidi kuwafundisha watoto wadogo kwa vitendo zaidi kwa kuwa wanachoka haraka na uwezo wao wa kumsikiliza mwalimu ni mdogo,hivyo kuwafundisha kwa njia ya vitendo kunawasaidia kulipenda somo na kuelewa kwa urahisi zaidi.Muhtasari huu umeundwa  kwa kuzingatia Sera ya elimu ya awali.Muhtasari wa Elimu ya Awali kwa shule za msingi(2005)umegawanyika katika vitendo vya masomo sita ambavyo ni:

 • Sehemu ya kwanza ni vitendo vya kujiunzia kiswahili.
 • Sehemu ya pili English Learning Activities
 • Sehemu ya tatu ni vitendo vya hisabati
 • Sehemu ya nne ni vitendo vya sayansi
 • Sehemu ya tano ni vitendo vya haiba na michezo
 • Sehemu ya sita ni vitendo vya sanaa

Katika kila aina ya vitendo vya masomo vipengele vifuatavyo vimeonyeshwa:malengo ya kufundisha vitendo hivyo,mada kuu na mada ndogo mbalimbali,malengo mahsusi ya kufundishia mada ndogo,mbinu mbalimbali za  kufundishia na kujifunzia pamoja na vifaa/Rejea za kufundishia na kujifunzia mada hizo .mwalimu wa elimu ya awali anatakiwa kutambua kuwa muhtasari huu umeundwa na masomo ambayo yameandikwa katika vitendo na yanafundishwa kwa vitendo.pia maudhui yake yameandikwa kwa kuzingatia malengo na umuhimu wa elimu ya awali kwa watoto wadogo.

Vitabu vya kiada na ziada

Vitabu vya kiada na ziada ni muhimu katika ufundishaji na ujifunzaji wowote.vitabu vya kiada hutumiwa    na watoto darasani sambamba na muhtasari wa mwalimu,vitabu vya kiada vya elimu ya awali vina maudhui ambayo yameandikwa kwa kuzingatia muhtasari wa vitendo vya masomo wa elimu ya awali.Maudhui katika kitabu cha kiada yanaweza kuelezwa njia ya picha na michoro.Pia kinaonyesha mbinu na mazoezi mbalimbali yanayohusu mada iliyofundishwa ambayo yamewekwa mwishoni mwa kila mada ndogo au vitendo vulani.Mambo mengine yaliyomo katika kitabu cha kiada ni utangulizi ambao unaonyesha ni watoto wa umri gani watatumia kitabu hicho.

Vitabu vya ziada vina maudhui ambayo yanafanana na yale ya muhtasari japokuwa yanaweza kuwa yameelezwa kwa undani zaidi au kidogo zaidi kulingana na kila mwalimu anachohitaji.Mwalimu anaweza kutumia vitabu vya ziada zaidi ya kimoja kufundishia mada fulani.Vitabu vya ziada ni muhimu sana kwa sababu vinamsaidia mwalimu kufundisha kwa ufanisi zaidi na pia vinamwongezea mwalimu maarifa na ujuzi zaidi.

Vitabu vya elimu ya awali vinatakiwa kuwa na sifa mbalimbali ambazo ni pamoja na maandishi makubwa ilikumwezesha mtoto kusoma kwa urahisi,picha kubwa zenye rangi nzuri zinazomvutia mtoto pamoja na jalada imara la kuvutia.Inafaa vitabu vya elimu ya awali viwe na kurasa chache ili visimchoshe mtoto.

Kiongozi cha mwalimu
kiongozi cha mwalimu ni kitabu kinachotoa mwongozo wa maelekezo kwa mwalimu wa elimu ya awali na jinsi ya kufundisha mada mbalimbali zilizopo katika muhtasari wa elimu ya awali.kitabu hiki kinamsaidia mwalimu kuwa na mtiririko mzuri katika kufundisha na hivyo kufundisha kwa ufanisi zaidi,hii ni kwasababu kinaonyesha hatua mbalimbali za somo kama mbinu za kufundishia mada fulani na majibu ya maswali yaliyoulizwa kwenye kitabu cha mwanafunzi au kitabu cha kiada.

Kitabu cha rejea
Hiki ni kitabu ambacho  kina baadhi ya mada ambazo ziko kwenye muhtasari lakini si mada zote zilizomo katika muhtasari ziko pia kwenye kitabu cha rejea.kulingana na tofauti za ujuzi na staili za uandishi,baadhi ya mada zinaweza kuwa zimeelezwa vizuri na kwa ufasaha zaidi katika kitabu cha rejea kuliko kitabu cha kiada,hivyo mwalimu huwaagiza wanafunzi kutumia kitabu hicho katika mada ambazo ameona zinafaa zaidi ili kuimarisha maarifa na ujuzi wa wanafunzi katika mada husika.
Kwa kila somo mwalimu anaweza kutayarisha orodha ndefu ya vitabu vya rejea kutegemea na upatikanaji wake katika mazingira ya shule.

Zana/vifaa vya kufundishia na kujifunzia
Hivi ni vitu ambavyo humsaidia mwalimu au mwanafunzi katika ufundishaji na ujifunzaji.Navyo vimegawanyika kitika zana za kujifunzia na kufundishia na vifaa vya kufundishia na kujifunzia.
Zana za kufundishia na kujifunzia ni kitu chochote kinachoweza kumsaidia mwalimu kufikisha ujumbe kwa wanafunzi kwa kuona kutenda au kusikia kutegemea na aina ya ujumbe unaotarajiwa kufundishwa mfano mawe, matunda mbalimbali kuwasilisha majina.
Kifaa cha kufundishia na kujifunzia ni kitu chochote ambacho mwalimu  na mwanafunzi hutumia ili kufanikisha tendo la kujifunza,mfano mishumaa katika kuwakilisha dhana ya joto au mwanga katika vitendo vya sayansi.
Ieleweke wazi pia kuwa kifaa hutegemea sana asili ya matumizi yaliyokusudiwa vinginevyo kifaa hicho chaweza kuawa zana pia.

UTAYARISHAJI WA MTAALA WA ELIMU YA AWALI

Mtaala wa elimu ya awali kama mitaala mingine hutayarishwa na Taasisi ya Elimu ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa elimu kama vile waalimu kwa kufuata hatua zifuatazo:

 • Kukusanya maoni juu ya mahitaji ya kujifunza ya watoto
 • Kuandaa malengo na kuteua mada zitakazofundishwa  kwa kushirikiana na wadau wa elimu mfano waalimu na maafisa wengine wenye uzoefu.
 • Kubainisha mbinu zitakazotumika katika kufundishia na kujifunzia
 • kubainisha zana na vifaa vitakavyotumika katika kufundishia na kujifunzia
 • Kubainisha vigezo na mbinu zitakazotumika katika upimaji na tathmini  ili kujua maendeleo ya ufundishaji na ujifunzaji.
 • Kufanya majaribio ya mtaala katika shule chache ili kupata ubora na upungufu wa mtaala huo kutokana na maoni ya watumiaji (waalimu na watoto)na kuuboresha zaidi kwa kuzingatia maoni hayo
 • Kuendesha mafunzo ya walimu kuhusu utumiaji wa mtaala huo
 • Kueneza utumiaji wa mtaala huo nchi nzima

UCHAMBUZI WA MTAALA WA ELIMU YA AWALI

Uchambuzi wa mtaala wa elimu ya awali ni muhimu kwa mwalimu ili kumsaidia katika maandalizi ya ratiba ya masomo,azimio la kazi,na andalio la somo

Uchambuzi wa mtaala wa elimu ya awali huhusisha maeneo muhimu yafuatayo:

 • vifaa/Zana za kufundishia na kujifunzia na upatikanaji wake
 • Kubainisha mada kuu na mada ndogo,na malengo mahsusi kwa kila mada ndogo
 • Kubainisha malengo ya jumla ya somo na malengo mahsusi kwa kila mada ndogo na kuona kama yanahusiana

  Uchambuzi wa mtaala wa elimu ya awali huhusisha uchambuzi wa mada mbalimbali zilizomo katika vitendo vya masomo

   Mtaala wa elimu ya awali hujumuisha masomo yafuatayo:

 

 1. Vitendo vya kujifunzia kiswahili
 2. English learning Activities
 3. vitendo vya hisabati mfano kujumlisha na kutoa namba zenye tarakimu moja
 4. Vitendo vya sayansi -watoto hujifunza dhana mblimbali za sayansi
 5. Vitendo vya haiba na michezo
 6. Vitendo vya sanaa-humsaidia mtoto kujifunza sanaa za aina mbalimbali

    UTEKELEZAJI WA MTAALA WA ELIMU YA AWALI

Mtaala wa elimu ya awali hutekelezwa chini ya usimamizi wa serikali  kama illvyo katika mitaala mingine.Baadhi ya matatizo makubwa katika utekelezaji wa mtaala ni pamoja na haya yafuatayo:

 • Upungufu wa vifaa na zana za kufundishia na kujifunzia elimu ya awali mfano vitabu vya kiada na ziada
 • Upungufu wa waalimu wenye mafunzo maalumu ya kufundishia elimu ya awali
 • Mazingira duni ya kufundishia na kujifunzia elimu ya awali mfano baadhi ya shule za awali zimefunguliwa katika nyumba za kawaida katika makazi ya watu,ambazo hazikubuniwa kwa madarasa ya watoto wadogo
 • Ukosefu wa viwanja vya kuchezea katika shule nyingi za awali hasa zile zinazoendeshwa na watu binafsi

MBINU ZA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA ELIMU YA AWALI.

Mbinu za kufundishia na kujifunzia ni mpango maalumu ambao mwalimu amebuni kuhusu uendeshaji wa somo lake,mpango huu hujumuisha mambo yafuatayo:
-Jinsi watoto watakavyojifunza
-Vitendo watakavyofanya
-Maswali atakayouliza na jinsi yatakavyojibiwa
-Mpango mzima wa uendeshaji wa somo na tathmini yake.

Watoto wa Elimu ya awali wanajifunza kwa kuangalia na kuiga wengine,kwa kujaribu na  kugundua,kwa kushughulika na vitu halisi na kwa kuchezea.Wanajifunza kama sehemu ya kukua kwao kwa ujumla kunakojumlisha kiakili,kimwili na kijamii.mtoto anajifunza zaidi kwa kushirikishwa.

Yafuatayo ni muhimu yawepo ili mtoto ajifunze vizuri zaidi:

-Viwepo vifaa vya kutosha kwa kila mtoto

-Mtoto awezeshwe kutumia vifaa hivyo kwa lengo la kujifunza dhana fulani iliyokusudiwa

-Mtoto apewe uhuru wa kuamua namna ya kucheza na vifaa hivyo

-Lugha/Msamiati unaotumika na watoto ni muhimu uwe rahisi kwa ajili ya mawasiliano ya watoto.

-Msaada kutoka kwa mwalimu usaidie juhudi za mtoto katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

AINA ZA NJIA ZA KUFUNDISHIA NA KUJIFUNZIA ELIMU YA  AWALI

Zipo njia kuu mbili za kufundishia/kujifunzia elimu ya awali

 

 • Njia ya maelekezo
 • Njia ya vitendo

Pia kuna njia nyingine mbili ambazo hutumika katika kufundishia darasa la awali ambazo ni

 • Njia huria
 • Njia ya mwega

Tukianza na njia ya maelekezo,katika njia hii mwalimu hufanya yafuatayo:

-Wanafunzi hufundishwa kwa njia ya maelekezo na maelezo mafupi
-Mwalimu huchagua vifaa vya kufundishia
-Anaelekeza jinsi ya kucheza navyo na matokeo yake katika kujifunza
-Mwalimu huulizwa maswali na kuwasifu watoto pale wanapotoa majibu sahihi na hata
wanapojaribu ili kuwapa motisha ya kujifunza
-Watoto husikiliza na kufuata maelekezo
-Majadiliano yanakuwa machache na watoto nafasi kidogo ya kuwa wabunifu

MANUFAA YA NJIA YA MAELEKEZO
-Ni nzuri kwa kufundishia maarifa mapya kwa watoto
-Utumiaji wa njia hii kwa watoto wa elimu ya awali ni lazima uzingatie mada tu ambazo watoto
hawawezi kujifunza kwa njia ya vitendo, nyimbo na hadithi ni mbinu ambazo huwavuta zaidi watoto

Njia ya Vitendo

Katika njia hii  watoto hufanya vitendo zaidi kama vile kufinyanga vitu,kuchezea vifaa mbalimbali vilivyoandaliwa,kusimulia hadithi,nyimbo na michezo mingine.
Vitendo hivi hufanyika chini ya ubunifu na usimamizi wa mwalimu na huwa na malengo maalumu ya kujifumza.
Watoto huelewa zaidi wanapojifunza kwa njia hii kwa vile watoto hutumia milango mingi zaidi ya fahamu katika kujifunza,njia hii pia ni nzuri katika shule ambazo ni rahisi kupata vifaa vya kila aina.

Njia huria

Katika njia hii mwalimu huandaa mazingira na vifaa vya kujifunzia na bila kuwaongoza watoto nani achezee nini  na ni vipi!watoto kufuatana na vipaji na mapenzi yao huchagua wenyewe  ni vifaa vipi vya kuchezea watumie katika tendo la kujifunza.ili kufanikisha hayo mwalimu anashauliwa kufanya yafuatayo:
-Kuwacha watoto wacheze na vifaa vya kuchezea kwa uhuru
-Kutowapangia watoto ratiba,kuweka mpangilio na vifaa vya kufundishia na michezo ya watoto
-Kuongea na watoto wanapouliza maswali na wanapotoa taarifa
-Kutoweka mpango maalumu darasani na kutoonyesha mwelekeo wa kuona watoto wanafanya kitu                      gani

Njia hii ina faida zifuatazo
-Njia hii inafaa kwa watoto wanaojiamini na wanaoweza kujua jinsi ya kutumia muda
-Aidha hutoa nafasi kwa mwalimu kuwasaidia watoto wanaohitaji  msaada wake.

Mapungufu ya njia huria ni haya yafuatayo:

 • Inaweza kuleta vurugu na kushindwa kulitawala darasa
 • Watoto wanaweza kuwa waharibifu hasa kama hawajui cha kufanya
 • watoto watakaoona hakuna cha kufanya wanaweza kukatishwa tamaa
 • Si rahisi kukidhi mahitaji vifaa na mazingira yatakayo mvutia kila mtoto

Njia ya mwega
Njia hii ni mchanganyiko wa njia mbalimbali yaani njia ya maelezo,njia huria na njia ya vitendo katika uwiano ambao mwalimu kama mtaaluma ataona unafaa.Ilikufanikisha hayo mwalimu hufanya yafuatayo:
-Hutumia njia zote kwa usawa
-Huweka mpangilio mzuri wa vitu darasani na kufuatilia kujifunza kwa watoto na mpango wa somo.
-Anawasaidia watoto kujifunza kwa kadili ya mahitaji yao

Njia hii inamanufaa kwa kuwa
-Watoto wanajisikia huru kujifunza kwenye mazingira yao
-Watoto wanjisikia kuthaminiwa,kusaidiwa na kusaidiana
-Katika mazingira haya watoto wanajenga kujiamini,uhuru na kufurahia kazi wanazozifanya.

MBINU ZA KUFUNDISHIA ELIMU YA AWALI

Njia za kufundishia na kujifunzia elimu ya awali ni utaratibu unaofuatwa ili kumwezesha mwalimu kufikisha ujumbe wake kwa watoto juu ya mada iliyopangwa.

Mbinu za kufundishia ni vitendo vilivyobuniwa ambavyo mtoto atafanya wakati wa mchakato wa tendo la kujifunza.Ubora wa matumizi ya njia hutegemea ubora wa mbinu zitakazotumika katika njia hiyo.Njia nzuri yaweza kuharibiwa na mbinu zisizofaa na hivyo kushindwa kujenga dhana iliyokusudiwa.

Mambo yanayompasa mwalimu wa shule ya awali ayafanye:

 • Kuwathamini watoto pamoja na kile wanachokifahamu.
 • Kuelewa na kuzingatia mapenzi ya watoto katika kujifunza,hivyo kuwapa nafasi kuchagua wanachokipenda.
 • Kufundisha kadri ya uelewa wa watoto.

Njia mbalimbali za kumsaidia mtoto katika kujifunza

 • Mwalimu aandae mazingira ili mtoto aweze kujifunza.
 • Watoto wapewe fursa ya kuchagua aina ya michezo wanayoitaka kutokana na vifaa mbalimbali ulivyowaandalia.
 • Watoto watumie muda mwingi kucheza/kujifunza peke yao au katika vikundi vidogo.
 • Watoto wapewe vitu halisi vya kuchezea kulingana na mazingira yao.
 • Mwalimu atoe msaada katika ili kufuatilia ushiriki wa wanafunzi kwa kuwauliza maswali au kuongeza vifaa vingine zaidi ya kuongeza ufahamu.
 • Mwalimu akubali kuwa kuaweza kuwa na jibu zaidi ya moja na watoto wanajifunza kwa kujaribu na kwa kukosea

Uandaaji wa mazingira ya kufundishia/kujifunzia
Dhana ya mazingira ya kufundishia na kujifunzia.
Mazingira ni vitu vyote vinavyotuzunguka.Tunaweza kuwa na mazingira ya aina tatu shuleni

 1. Mazingira halisi kwa mfano mpango wa chumba,nafasi,samani
 2. Mazingira ya shughuli kama vile mpango wa ratiba
 3. Mazingira ya kihisia,kwa mfano mielekeo na hisia za watu.

Tukianza na mazingira halisi haya hujumuisha mambo yafuatayo:
Mpango wa chumba,samani,vifaa,hali ya joto,usafi, rangi,stoo,eneo la maonyesho,utunzi,nafasi ya ndani,nafasi ya nje,kelele,nuru,sakafu,salama,vyoo,madilisha na milango,sehemu za shughul.

Mwalimu anawajibika kuandaa mazingira halisi yanayofaa kiafya kiusalama na ambayo yatasaidia kujifunza.

Ilimpango chumba uwe wa kufaa;

 • Andaa meza na viti kwa shughuli zinazohitaji kukaa.
 • Andaa nafasi ya sakafu kwa ajili ya kuchezea,unaweza kutumia mikeka na vifaa vingine vya ubunifu
 • Andaa sehemu za wazi kwa ajili ya shughuli ya makundi makubwa
 • Kuwepo nafasi ya watoto kupita bila kuwasumbua wenzao
 • Kama shughuli inahusisha kikundi ni muhimu kupanga viti katika hali ya duara ili kuruhusu mawasiliano chanya kati ya mwalimu na watoto au watoto wenyewe kwa wenyewe.

Mambo muhimu kuhusu vifaa:

 • Weka vifaa na wanasesere mahali ambapo watoto wanaweza kuchukua na kurudisha wenyewe.
 • Weka vifaa na (vifani)wanasesere karibu na mahali watakapotumia.
 • Hifadhi vitu vya hatari mahali mbali na watoto

Vituo vya shughuli

Vituo vya shughuli ni sehemu zilizowekwa vitu mbalimbali vya kuvutia.Ilivituo vya shughuli viweze kufaa vinahitaji mambo yafuatayo;

 

 • Gawa chumba kwenye sehemu za vivutio mbalimbali
 • Tenga shughuli zenye kelele na zile zinazohitaji ukimya.
 • Panga vituo hivyo ili watoto waweze kufanya shughuli kwa vikundi

Ifuatayo ni mifano ya vituo vya shughuli:

 

 • Meza ya hisabati
 • Jukwaa la vikaragosi
 • Michezo ya chemsha bongo na michezo mingine.
 • Mahali pa kusomea
 • Meza ya sayansi
 • Kona ya maktaba
 • Kituo cha kuandikia
 • kituo cha utunzaji nyumba
 • Kituo cha sanaa na ufundi
 • Kona ya ujenzi

Baadhi ya mambo muhimu kuhusu nafasi ya nje

 • Andaa nafasi ya wazi ili watoto waweze kukimbia na kutembea kwa uhuru
 • Andaa vifaa vinavyosaidia ukuaji wa kimwili,kwa mfano vifaa vya michezo ya kukwea,kuruka,kuninginia,na bembea.
 • Andaa vifaa muhimu vya kucheze
 • Andaa nafasi ya sanaa na ufundi

Sehemu ya maonyesho

 • Andaa sehemu za maonyesho ya kazi za watoto
 • Andaa nafasi ukutani kuonyesha picha,chati na maneno
 • Andaa meza ya kuonyesha vitu halisi,vifaa vya sayansi n.k.
 • Iweke sehemu ya maonyesho katika hali ya kuvutia na kuwahamasisha watoto kujifunza.

Mazingira ya kihisia
Mazingira ya kihisia hufanywa na mambo muhimu yafuatayo;

 • Mwelekeo wa mwalimu
 • Tabia ya mwalimu
 • Utaratibu wa mawasiliano na mahusiano baina ya mwalimu na watoto
 • Mahusiano na wazazai
 • Mahusiano ya mtoto na mtoto
 • Utaratibu au sheria za kinidhamu zilizowekwa shuleni

Mwalimu anaowajibu wa kuandaa mazingira ya kihisia yanayovutia na yanayomsaidia kila mtoto kujisikia vizuri na kufurahia kuwepo shuleni..Mtoto anapaswa awe huru kuchunguza,kudadisi,kuuliza maswali na kujifunza.Ili mtoto aweze kuupata uhuru huo,mwalimu azingatie yafuatayo:

Usawa
Walimu wawatendee watoto wote kwa uangalifu na heshima na wasiwabague kwa misingi ya
jinsi,utaifa,dini au ukabila.

Tofauti ya uwezo wa watoto na matatizo ya kujifunza.
Walimu wamtambue kila mtoto kuwa ni mtu binafsi mwenye kipaji,mahitaji,hisia,hitilafu na vivutio
vinavyoweza kutofautiana na watoto wengine.Hivyo kila mtoto atendewe kadri ya mahitaji yake
yanavyoonyesha.

Ushirikiano
Walimu wafanye kazi pamoja na kushirikiana na walimu wengine,wafanyakazi wengine na wazazi
kwa manufaa ya wanafunzi na shule.

Nidhamu
Walimu kamwe wasitumie adhabu za vipigo,kauli za matusi au vitisho kudhibiti tabia za watoto.
Wawaongoze watoto kujifunza na kuelewa sheria na mipaka ya shule na kufuata tabia zinakubalika
katika jamii.

Uandaaji wa somo
Uandaaji ni ufunguo wa mipango yenye mafanikio kwa watoto.shughuli illiyopangwa vizuri itatekel
ezwa vizuri,watoto watajishughulisha na watafurahi,na Mwalimu ataona malengo yake kwa watoto
yamefikiwa

Upangaji mzuri huhitaji mwalimu afikiri mapema.kiasi mwalimu anavyopanga na kutayarisha ma-
pema,ndivyo atakavyokuwa na kazi nyepesi wakati wa ufundishaji.Hali hii itampa nafasi ya kuzung
umza na kushughulika na watoto.

Hatua za uandaaji wa somo

 • Bainisha malengo unayotaka kufikia ukitofautisha lengo kuu na malengo mahsusi
 • Bainisha shughuli za kujifunza ukizingatia malengo mahsusi.
 • Andaa vifaa na nafasi kabla ya kuanza somo
 • Hakikisha shughuli inawavutia watoto.
 • Fanya mazoezi kabla ya wakati wa kufundisha kama inawezekana
 • Tekeleza shughuli ulizopanga ipasavyo.Endesha shughuli kwa namna  itakavyowavutia watoto na kuwafanya waelewe
 • Wasaidie watoto kwa kiasi fulani tu,waache wawe huru katika kujifunza kwao,kwa kiasi inavyowezekana.
 • Sughulika na wanafunzi kusafisha na kurudisha vifaa,hii ni muhimu sana katika kuwafundisha kuwajibika.

Tathmini

Katika kutathmini mipango yako jiulize maswali yafuatayo;

 • Je umefikia malengo yako?
 • Je watoto wamejifunza ulichokusudia?
 • Unajuaje kuwa umefikia malengo ya somo?
 • Watoto walifurahia shughuli au somo?
 • Ni vipi ungeweza kufanya shughuli iwe nzuri zaidi wakati mwingine?
 • Je shughuli ililingana na kiwango cha watoto au ingeweza kurekebishwa?
 • Wakati wa shughuli je uliona mtoto yeyote anahitaji msaada wa ziada au uangalizi maalum,au alionyesha uwezo wa pekee?
 • Je ni maeneo yapi yaliwapa watoto ugumu wa kujifunza?

Mitihani katika shule ya awali
Utafiti umeonyesha ya kuwa mitihani haina usahihi katika kupima watoto wa shule za awali.Si sahi-
hi kwasababu watoto hawaelewi dhana ya kupimwa.Pia mitihani mingi haipimi uwezo halisi wa wa
toto kwasababu mara nyingi mtoto haonyeshi anachojua kwenye mtihani.
Mitihani haifai pia kwa sababu inashawishi tulinganishe alama za mtoto mmoja na mwingine.Kwa
kuwa watoto hukua kwa hatua tofauti,ulinganisho huo hautoi dhana sahihi.
Alama za mtoto za mtihani si kigezo pekee cha kutabiri utendaji wake shuleni miaka ya baadaye.
Utendaji wake shuleni baadaye utategemea stadi za kujieleza kujiamini,stadi za kufikiri na uwezo
wa kushirikiana na wenzake.

Maendeleo ya mtoto yapimwe kwa uchunguzi wa mwalimu wa mwaka mzima na sio kwa mtihani
Maendeleo ya watoto yalinganishwe na ya wakati uliopita sio na watoto wengine.
Matokeo ya upimaji wa maendeleo ya watoto yatumiwe kupanga utaratibu wa kujifunza baadaye.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s